Ndoto ya klabu ya Yanga sc kucheza fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika imefika mwisho baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 kwa penati baada ya matokeo ya 0-0 dhidi ya Mamelod Sundowns ya nchini Afrika kusini.
Mchezo huo wa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika ilifanyika katika uwanja wa Loftus Verfied jijini Pretoria ambapo katika mchezo wa awali jijini Dar es salaam timu hizo zilitoka suluhu na katika mchezo wa pili pia timu hizo zilisuluhu katika dakika 90 na mwamuzi kuamua hatua ya matuta kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la soka barani Afrika (Caf).
Vikosi vya timu zote vilikua na mabadiliko machache kutoka katika vikosi vya mchezo wa kwanza jijini Dar es salaam ambapo Yanga sc walimuanzisha Joseph Guede badala ya Clement Mzize na Mamelod Sundowns walimuanzisha nahodha Themba Zwane na kumuweka benchi Gasto Sirino.
Yanga sc waliingia na mfumo wa kujilinda zaidi wakishambulia kwa kushtukiza na nusura waape mabao kupitia kwa Guede,Musonda na Aziz Ki ambaye bao lake lilionekana halali lakini lilikataliwa na mwamuzi msaidizi wa Video (VAR) ambapo kwa mujibu wa picha za marejeo mpira uliingia golini.
Mpaka dakika 90 zinakamili mchezo uliingia hatua ya matuta na Aziz Ki,Dickson Job na Ibrahim Hamad walikosa matuta haya ambapo kipa Ronwell Williams alidaka huku Bacca akipaisha penati ya mwisho na safari ya Yanga Sc kimataifa kuishia hapo.
Mamelod sasa inasubiri mshindi kati ya Asec Mimosa na Esperance De Tunis ili kujua itakutana na nani katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.