Baada ya kupata sare ya 1-1 dhidi ya Al Ahly kikosi cha klabu ya Yanga sc kimetua salama nchini Ghana tayari kwa mchezo wa tatu wa ligi ya mabingwa dhidi ya Medeama Fc ya nchini humo utakaofanyika siku ya ijumaa Disemba 8 nchini humo.
Yanga sc imewasili ikiwa na matumaini makubwa ya kupata alama tatu ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo ambayo ilishindwa kufuzu hatua ya makundi kwa zaidi ya miaka 25.
Kocha Miguel Gamondi amesema kuwa maandalizi ya kikosi hicho tayari yamekamilika na sasa hawana cha kupoteza zaidi ya kupata alama tatu muhimu huku akiahidi kurekebisha makosa katika michezo miwili iliyopita.
“Pointi moja tuliyopata tumeivujia jasho haikuwa rahisi hivyo zinahitajika mbinu zaidi kuelekea mchezo wetu na Medeama ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele” amesema Gamondi
“Makosa tuliyoyafanya hayawezi kujirudia tulikuwa bora dhidi ya CR Belouizdad tukapoteza kwa idadi kubwa ya mabao tukatulia na kusawazisha makosa kwenye mchezo uliofuata tumepata pointi moja baada ya sare mchezo unaofuata utakuwa mgumu lakini malengo ni pointi tatu.” amesema.
Gamondi ameongeza hakuna lisilowezekana kama watafanya maandalizi ya kutosha na kujiandaa vyema kuikabili Medeama huku akikiri kuwa amekaa na wachezaji wake kuwaeleza kuwa kila mchezo ulio mbele yao sasa ni fainali.
Yanga sc mpaka sasa ina alama moja mkiani mwa kundi D huku ikitakiwa kushinda mchezo huo ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu dhidi ya timu za Al Ahly,CR Belouzdad na Medeama Fc.