Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika baada ya kuifunga Cr Belouzdad ya nchini Morocco kwa mabao 4-0 katika mchezo wa mzunguko wa tano wa Kundi D uliofanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
Yanga sc baada ya kupata ushindi huo sasa imefikisha alama nane katika nafasi ya pili ya kundi D huku Al Ahly ikiwa kileleni na alama tisa na Belouzdad yenyewe ipo nafasi ya tatu na alama tano huku Medeama ikiwa mkiani na alama nne na kila timu imesaliwa na mchezo mmoja mmoja.
Yanga sc ilihitaji ushindi wa mabao hayo ili kufuzu moja kwa moja pasipo kutegemea matokeo ya mchezo wa mwisho dhidi ya Al Ahly ugenini nchini Misri ambapo baada ya kupata ushindi huo sasa ni moja kwa moja wamefuzu kwa mujibu wa kanuni za Caf ambapo baada ya timu kulingana alama basi huangalia matokeo baina ya timu mbili zilipokutana (Head to Head).
Mudathir Yahya ameendelea kuwa mchezaji muhimu kwa Yanga sc baada ya kufunga bao la uongozi dakika chache kabla ya mapumziko akiunganisha kwa shuti kali krosi kutoka kwa Joyce Lomalisa Mutambala na kuzua shangwe kwa mashabiki wa Yanga sc huku Stephane Aziz Ki akifunga bao la pili dakika ya 46 mapema kipindi cha pili baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Belouzdad.
Pacome Zouzou ambaye siku hiyo ilipewa jina lake na mashabiki kulazimika kupaka nywele rangi ili kufanana na rangi ya nywele ya mchezaji huyo alifanya kufuru baada ya kuwazisi maarifa mabeki wa Belouzdad pamoja na kipa kisha kumpasia mpira Kennedy Musonda ambaye alifunga bao la tatu kwa Yanga sc.
Pengine Yanga sc ingeibuka na ushindi mkubwa zaidi kama Aziz Ki na Pacome wangetumia vizuri nafasi walizopata mapema zaidi lakini iliwapasa kusubiri mpaka dakika ya 84 kupata bao la nne kupitia kwa Joseph Guede ambaye alipokea pasi nzuri ya Aziz Ki na kufunga bao hilo liliwapa Yanga sc tiketi ya kuingia robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.