Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kupata udhamini mnono wa miaka mitano kutoka kampuni ya Gsm Beverages ya jijini Dar es salaam inayojihusisha na kuuza vinywaji ikiwemo vya kuongeza nguvu sambamba na maji ya kunywa ambapo mkataba huo umesaini mapema leo jijini Dar es salaam.
Mkataba huo wa miaka mitano una thamani ya kiasi cha shilingi bilioni moja ambapo Yanga sc itapata kiasi cha shilingi milioni mia mbili kila msimu kwa kipindi chote cha mkataba huo ambapo maji ya kunywa ambayo yatatumiwa na timu hiyo kuanzia sasa ni yale yanayotengenezwa na kampuni hiyo huku wakiweka tangazo nyuma ya jezi za klabu hiyo kuanzia msimu huu.
Mkataba huo umesainiwa mbele ya waandishi wa habari ambapo klabu ya Yanga sc iliwakilishwa na Mkurugenzi wa sheria wa klabu hiyo Simon Patrick huku Gsm ikiwakilishwa na Mkurugenzi wake mkuu Mr.Benson Mahenya.
“Leo tumekuja hapa kuwatangazia wadhamini wetu kuelekea kilele cha wiki ya Mwananchi, mdhamini mkuu wa wiki ya mwananchi ni benki ya CRDB, hata hivyo tumeongeza washirika wengine ni Benki ya Equity pamoja na GSM Beverage” Simoni Patrick Mkurugenzi wa Sheria Klabu ya Yanga SC akiwatambulisha wadhamini wapya klabuni hapo.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Gsm aliwashukuru Yanga sc kwa fursa hiyo huku akiwaahidi kutimiza yale yote waliyokubaliana katika mkataba huo wa miaka mitano.
“Kwa niaba ya GSM Group tunayo furaha ya kutangaza rasmi kuwa tumepanua wigo wa mahusiano yetu na klabu ya Yanga SC, tunatangaza rasmi kuwa kampuni mpya ya vinywaji ya GSM imeingia mkataba wa miaka mitano na klabu ya Yanga SC, na mkataba huu una thamani ya Tsh bilion 1” Alisema Benson Mahenya ambaye ni Afisa Mtendaji mkuu wa GSM Group.
Yanga sc imebahatika kuwa na mvuto mkubwa kibiashara kutokana na kufanya vizuri uwanjani kwa kipindi cha miaka mitatu sasa ambapo imekua na makampuni mengi yanyoidhamini klabu hiyo kuanzia Gsm,Crdb,Aghakhan Hospital na wengine wengi.