Uimara wa Kipa Loy Matampi umeifanya Yanga sc kuibuka na ushindi kiduchu wa 1-0 dhidi ya Coastal Union kutoka jijini Tanga katika mchezo wa ligi kuu ya soka ya Nbc uliofanyika katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es salaam.
Yanga sc ikizidi kujichimbia kileleni baada ya ushindi huo kupitia bao la Joseph Guede dakika ya 76 ya mchezo akimalizia pasi safi ya Kennedy Musonda ambaye alipokea mpira wa Yao Kouasi Attohoula ambaye alipiga krosi safi kwenye eneo la kumi na nane.
Kipa Loy Matampi alionyesha umahiri kuzuia michomo ya Stephane Aziz Ki,Joseph Guede,Kennedy Musonda pamoja na Mudathir Yahya kiasi cha mashabiki wa Yanga sc kuanza kupata hofu kuwa huenda wakapata sare ya pili mfululizo baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya JKT Tanzania.
Coastal Union wakicheza kwa tahadhari ya kuepuka kufungwa mabao mengi muda mwingi walikaa nyuma wakizuia huku wakishambulia kwa kushtukiza jambo ambalo liliwagharimu baadhi ya nyakati kutokana na Yanga sc kuweka presha kubwa katika kushambulia na kusababisha mlinzi Lameck Lawi kupata kadi nyekundu baada ya kumvuta Aziz Ki dakika ya 70 akielekea kufunga.
Sasa Yanga sc imefikisha alama 62 katika michezo 24 ya ligi kuu huku Azam Fc ikiwa katika nafasi ya pili na alama 54 na Coastal Union imesalia katika nafasi ya nne ikiwa na alama 33 ikimezewa mate na Kmc yenye alama 32 katika nafasi ya tano huku timu zikiwa na michezo 24 kila mmoja.