Msafara wa watu sitini wakiwemo wachezaji 24 na viongozi sambamba na benchi la ufundi la klabu ya Yanga sc unatarajiwa kuondoka mapema jioni ya leo kuelekea nchini Misri kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kundi D baina ya klabu hiyo na klabu ya Al Ahly ya nchini humo.
Mchezo huo wa mwisho utafanyika siku ya Ijumaa majira ya saa moja jioni kwa saa za Tanzania ambapo utaamua mshindi wa kwanza na pili wa kundi D ambapo tayari timu za Yanga sc na Al Ahly zimefuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika huku Medeama Fc na CR Belouzdad zikitolewa katika hatua ya makundi.
Yanga sc imepanga kushinda mchezo huo ambapo kocha Miguel Gamond amesema kuwa atacheza kwa kurelax ili kupata alama tatu muhimu na hatimaye kuongoza kundi D ili asipate timu ngumu katika hatua ya robo fainali ambapo pia atakua na faida ya kuanzia ugenini na kumalizia nyumbani.
“Nawafahamu Al Ahly vizuri kwa kuwa nimefundisha soka Afrika muda mrefu hivyo nawafahamu aina ya uchezaji wao naandaa timu kwenda kucheza kwa kurelax bila presha ili kupata matokeo kwenye mchezo huo tuweze kuongoza kundi”Alisema Gamond
Naye meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo alisema kuwa kikosi hicho kinaondoka mapema leo na kufika Misri saa saba usiku wa kuamkia kesho ambapo kitapitia nchini Ethiopia.
“Timu inatarajia kuondoka saa 11:55 jioni kuelekea Misri, tutaondoka na shirika la ndege la Ethiopia na kufika saa 2:33 usiku, kisha tutaondoka Ethiopia na kuwasili Cairo saa saba usiku kuamkia kesho. Timu itafikia Royal Kempinski Hotel.
Tutaondoka namsafara wa watu 60, msafara huu umegawanyika makundi matatu, wachezaji 24, benchi la ufundi 13, na Watendaji/maofisa wakuu wa klabu 23” Alisema Ali Kamwe Meneja Habari na Mawasiliano Young Africans SC.