Uwezo mkubwa wa kikosi cha Yanga sc iliounyesha katika mchezo wa kirafiki dhidi ya klabu ya Kaizer Chiefs umewaacha mashabiki midomo wazi nchini humo kutokana na kuwafunga wasauzi hao mabao 4-0 huku wakiwachezea mpira wa kikubwa pamoja na kuwa ugenini.
Yanga sc ilicheza mchezo huo ukiwa ni mchezo wa tatu wa kirafiki nchini humo ilipoenda kwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya ambapo pia ilipata nafasi ya kushiriki michuano maalumu ya Mpumalanga Cup ambayo Ts Galaxy ya nchini humo iliibuka mabingwa na pia ilishiriki mchezo mmoja wa Toyota Cup ambayo ilifanikiwa kutwaa kombe hilo.
Mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Toyota Free State uliwakutanisha makocha wenye mbinu nyingi Nasredine Nabi na Miguel Gamondi ambapo ilimlazimu Nabi kukubali kipigo hicho cha mabao 4-0 huku Prince Dube akifunga bao la kutangulia dakika ya 24 baada ya mabeki kuzubaa kuokoa mpira alioupiga yeye mwenyewe.
Stephane Aziz Ki alifunga bao zuri mwishoni mwa kipindi cha kwanza akipokea pasi ya Duke Abuya baada ya kumnyang’anya mpira beki wa Kaizer Chiefs na mpaka mapumziko matokeo yalikua 2-0.
Kipindi cha pili Yanga sc waliingia na kutia presha kubwa kwa wapinzani na kusababisha muda mwingi kutokua makini na kuingia katika mtego wa washambuliaji wa Yanga sc ambapo Prince Dube aliwazidi maarifa mabeki ya Kaizer n akufanikiwa kumpasia Clement Mzize aliyefunga bao la tatu dakika ya 56.
Dakika ya 62 makosa ya walinzi wa Kaizer Chief yalimzawadia Stephane Aziz Ki bao la nne baada ya beki kurudisha pasi fupi na Ki kuiwahi na kuwachambua kipa na walinzi wake na mabao hayo yalidumu mpaka mwisho mwa mchezo pamoja na jitihada za Ranga Chivaviro kujitahidi kufunga lakini alikua chini ya ulinzi mkali wa Ibrahim Bacca na Dickson Job.
Kocha Miguel Gamondi ni kama tayari ameshapata kikosi cha kwanza ambacho kilianza mchezo huo kikiwajumuisha Diarra,Yao,Kibabage,Job,Bacca,Aucho,Duke,Nzengeli,Mzize,Aziz Ki na Dube huku wachezaji walioingia kipindi cha pili ambao ni Chama,Pacome,Baleke na Mudathir wakiwa na uhakika wa kuanza ama kuanzia benchi.