Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imekubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Morocco katika mchezo wa kwanza wa kundi F uliofanyika katika mji wa San Pedro nchini Ivory Coast ambapo michuano hiyo inaendelea.
Stars ikiwa chini ya Mwalimu Adel Amrouche ilianza katika mchezo huo ikiwa na mabeki pamoja na viungo wengi wakiongozwa na Bakari Mwamnyeto,Ibrahim Hamad,Mohamed Hussein na Haji Mnoga sambamba na viungo Himid Mao,Novatus Dismass,Mudathir Yahaya huku eneo la mbele likimtegemea zaidi Mbwana Samata.
Kikosi cha Morocco kilichosheheni mastaa wengi kutoka ulaya kilifanikiwa kupata bao la uongozi dakika ya 30 likifungwa na Romain Saïss aliyamalizia mpira uliotemwa na kipa Aishi Manula na kumkuta mfungaji akiwa hajakabwa.
Kipindi pili hasa baada ya Novatus Miroshi kupata kadi nyekundu huku Mbwana Samata akitolewa ilisababisha Morocco kuuchukua mchezo na kupata mabao mawili ya haraka yakifungwa na Azzedine Ounahi na Youssef En-Nesyri yaliyohakikisha ushindi kwa wababe hao wa soka la Afrika kwa sasa.
Mbinu za kocha Adel Amrouche na uchaguzi wa wachezaji ni moja ya sababu kwa Stars kupoteza mchezo huo ambapo sasa wanashika mkia katika msimamo wa kundi F huku Morocco akiwa kileleni na Zambia pamoja na DRC Congo wakishika nafasi ya pili na tatu.