Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinakabiliwa na wakati mgumu kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Ivory Coast hasa baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Zambia katika mchezo wa raundi ya pili ya kundi F.
Katika mchezo huo Stars tayari walishauchukua baada ya kuwa wanaongoza kwa 1-0 huku Zambia wakiwa pungufu baada ya kiungo wao Rodrick Kabwe kupewa kadi nyekundu dakika ya 44 ya mchezo huku Stars wakipata bao la mapema kutoka kwa Simon Msuva aliyemalizia pasi nzuri ya Mbwana Samata dakika ya 11 ya mchezo.
Stars ilikosa umakini kuanzia kipindi cha pili baada ya Zambia kuwa na presha ya kupata ushindi ambapo walijisahau mara kwa mara na kupanda bila mpangilio huku wakiacha nafasi kadhaa za wazi kwa mastaa wa Stars kufunga kwa kutumia mashambulizi ya kushtukiza ambapo Stars walikosa nafasi kadhaa za magoli.
Kuingia kwa Cletous Chama na Kennedy Musonda kulitibua mipango ya Stars ambapo Zambia walitengeneza presha kubwa katika kushambulia na kufanikiwa kupata bao kupitia kwa Patson Daka dakika ya 88 ya mchezo bao ambalo lilitibua mipango ya Stars kufuzu hatua inayofuatia.
Tumaini pekee kwa Stars ni kumfunga Congo Drc huku wakiomba Morocco iwafunge Zambia katika mchezo wa mwisho ili kupata uhakika wa kufuzu hatua hiyo ya 16 bora kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo tangu Tanzania ishiriki ambapo sasa ni mara ya tatu.