Klabu ya Simba sc imepoteza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga sc siku ya Jumamosi baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 ikiwa ni mara ya pili katika mechi mbili za ligi kuu kwa msimu huu wa 2023/2024.
Yanga sc imefanikiwa kuifunga Simba sc mara mbili ikivunja rekodi yake ya miaka kumi ambapo mara ya mwisho kufanya hivyo ilikua msimu wa 2014/2015 ambapo kwa msimu huu jumla ya mabao 7-2 yamefungwa ambapo mchezo wa kwanza Yanga sc ilishinda 5-1 na mchezo wa pili 2-1.
Stephan Aziz Ki ambaye awali kabla ya kutua nchini alihusishwa na Simba sc alifunga bao la kwanza dakika ya 20 kwa penati baada ya kuangushwa na beki Hussein Kazi aliyekua akitaka kuokoa hatari baada ya Aziz kumpora mpira na kuingia nao ndani ya eneo la 18 na ndipo mwamuzi Ahmed Arajiga alipoamuru pigo la penati na kipa Ayoub Lakred alishindwa kuucheza mpira huo.
Simba sc licha ya kutawala mchezo dakika 15 za mwanzo walijikuta wanafungwa bao la pili baada ya Joseph Guede kuwahadaa walinzi wa Simba sc wakijua ameotea na kupokea pasi nzuri kutoka kwa Khalid Aucho na kufunga bao la pili na kuwaacha mashabiki wa Simba sc wakiwa hawaamini macho yao mnamo dakika ya 38 ya mchezo.
Mpaka mapumziko matokeo yalibaki 2-0 ambapo dakika ya 74 Simba sc walipata bao la kufutia machozi likifungwa na Fredy Michael akipokea pasi nzuri ya Cletous Chama na kuwazidi maarifa walinzi wa Yanga sc na kufunga.
Kocha Benchika alijitahidi kutumia kila namna kusawazisha mabao hayo ambapo aliamua kuwaingiza washambuliaji wake Fredy na Pa Omar Jobe pamoja na winga Luis Miqquisone kuja kuongeza nguvu lakini mpaka dakika 90 matokeo yalikua 2-1.
Yanga sc sasa imevuna alama 58 katika michezo 23 ya ligi kuu nchini ambapo Simba sc imesalia nafasi ya tatu ya msimamo ikiwa na alama 46 ikicheza michezo 21 ya ligi kuu.