Klabu ya Simba sc imeshindwa kuibuka na alama tatu baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu uliofanyika katika uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba mkoani Kagera na kuambulia alama moja pekee.
Sare hiyo imeiweka rehani nafasi ya pili ya ligi kuu baada ya Simba sc kuwa na wakati mgumu wa kuizidi Azam Fc licha ya kuifunga 3-0 katika mchezo ambao zilikutana zenyewe wiki iliyopita ambapo Simba sc ilipunguza pengo la alama tatu katika msimamo na kubaki moja.
Fred Minziro alichagua kuiheshimu Simba sc ambapo alijaza viungo wengi eneo la nyuma huku akiweka mabeki wanaopenda kukaba zaidi akiwemo Edwin Bukenya ambaye aliondoa hatari nyingi langoni mwa Kagera Sugar sambamba na Abdalah Seseme aliyekaba zaidi eneo la kiungo.
Fredy Michael aliikosesha Simba sc alama tatu baada ya kukosa bao la wazi mapema dakika za mwanzo za mchezo ambapo jitihada na utlivu wa Ladack Chasambi ziliipatia Simba sc bao dakika ya 24 ambalo lilisawazishwa na Obrey Chirwa dakika ya 64 akiunganisha kona baada ya mabeki wa Simba sc kuzembea kuiokoa.
Mpaka dakika tisini zinakamilika timu hizo ziligawana alama moja moja na Simba sc kufikisha alama 57 nafasi ya tatu ya msimamo huku Azam Fc ikifikisha alama 60 baada ya kuifunga Kmc 2-1 na kuishirikiria nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kuu ya Nbc.