Kocha wa klabu ya Kmc Abduhamid Moalin amevunja mkataba wa nafasi ya ukocha mkuu wa klabu hiyo kutokana na klabu kushindwa kutekeleza baadhi ya makubaliano ya kimkataba baina ya pande hizo.
Moalin aliyejiunga na Kmc msimu uliopita baada ya kuondoka Azam fc amewasilisha barua ya kuvunja mkataba kwa mabosi wa Kmc siku chache zilizopita ambapo ametaja sababu kadhaa kuhusu kuvunja mkataba huo.
Katika barua yake Moalin ametaja baadhi ya mambo ya kimkataba ambayo menejimenti ya klabu hiyo imeshindwa kuyatekeleza ni pamoja na kutomlipa baadhi ya stahiki zake za kimkataba pamoja na kushindwa kumpa gari la kutembelea lenye hadhi.
Pamoja na sababu hizo zipo taarifa zinazodai kuwa kocha huyo amelazimika kufikia uamuzi huo baada ya kufikia makubaliano na mabosi wa klabu ya Yanga sc kuwa kocha msaidizi wa klabu hiyo akichukua nafasi ya Mussa Ndaw ambaye ametimuliwa klabuni hapo.
Ndaw ambaye alikua msaidizi wa kocha mkuu Miguel Gamondi ametimuliwa kikosini humo kutokana na changamoto ya nidhamu hali iliyopelekea kikosi hicho kukosa nidhamu hasa ndani ya kambi ikiwemo kukosekana kwa Ushirikiano na wataalamu wenzake wa benchi la ufundi.
Mpaka sasa bado hakuna taarifa kamili kutoka upande wa Yanga Sc kuhusu suala hilo ambapo inasubiriwa kuona kama kuna taarifa rasmi kwa upande wa Yanga sc kwa siku mbili zijazo.