Klabu ya Yanga sc leo imeingia mkataba wa mwaka mmoja na kampuni ya Silver General Investment ambapo mashabiki wa klabu hiyo na Watanzania wote wanaweza kukopeshwa simu na kulipa kwa awamu tofauti kupitia utaratibu maalumu katika matawi ya klabu hiyo.
Mkataba huo umesainiwa mapema leo na Rais wa Yanga Sc Eng.Hersi Said pamoja na wawakilishi wa kampuni hiyo Jerry Onassa ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo.
“Mwanachama na Shabiki wa Young Africans ambaye anahitaji kukopeshwa simu anapaswa kutoa kiasi cha Tsh 75,000 na kiasi kinachobaki analipa kidogo kidogo. Ndani ya simu utapata App ya Yanga SC ambayo imelipiwa kwa miezi miwili na nusu. Natoa wito kwa Wanachama wa Young Africans SC kuikimbilia fursa hii ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Klabu yako”Alisema Hersi mbele ya waandishi wa habari.
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo Jerry Onassa aliipongeza klabu ya Yanga sc kwa kukubali kutumia fursa hiyo ya kuwapa faida mashabiki wa klabu hiyo kupata simu hizo ambazo zitasaidia kupata habari za klabu hiyo na kuwa chanzo cha mapato kwa klabu.
“Naipongeza Klabu ya Young Africans SC kwa mapinduzi haya ya kuthamini Wanachama na Mashabiki wake kwa kuwarahisishia mfumo mzuri wa wao kupata simu hizi za smartphone. Haya ni mapinduzi makubwa ya kidigitali kwa Klabu. Asanteni kwa kuungana nasi na tutawahakikishia kuwapa ushirikiano mzuri”Alisema Jerry.
Rais wa Yanga sc Eng.Hersi pia alieleza namna wataalam wa klabu hiyo watakavyofanya mchakato wa kurahisisha malipo na upatikanaji wa mikopo hiyo kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo “Wataalamu wetu wa Silver General Investment watatoa semina ya namna gani simu hizi za mkopo zinapatikana na zinapaswa kulipiwa. Kimsingi simu hizi hazitalipiwa kwa kutoa hela keshi. Watakuwa na mfumo maalum wa kulipia ili kuepukana na matapeli ambao wanaweza kuathiri biashara hii. Tutatumia matawi yetu kuratibisha mfumo mzima wa ukopeshwaji na ulipaji ili kudhibiti mwenendo mzima wa biashara hii”.
Simu hizo moja kwa moja zitakua zimeunganishwa na aplikasheni ya Yanga sc ambapo mnunuzi atapata faida ya kutumia kwa miezi miwili bila kulipia kwa kuwa itakua ishalipiwa na moja kwa moja.