Real Madrid wameendeleza ubabe dhidi ya FC Barcelona baada ya kuitungua kwa mabao 3-2 katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la super cup la Hispania uliofanyika huko Riyad Saudi Arabia.
Mabingwa hao wa kihistoria wa kombe la klabu bingwa Ulaya walio kwenye ubora mkubwa siku za hivi karibuni walishusha kikosi kamili uwanjani walifanikiwa kupata goli la kwanza dakika ya 25 kupitia kwa winga Vinicius Junior akipokea pasi ya Karim Benzema ambaye wametengeneza naye moja ya muunganiko bora barani Ulaya msimu huu.
Barca walirejea mchezoni na kusawazisha bao hilo dakika ya 41 kupitia kwa mshambuliaji Luuk De Jong akitumia vema makosa ya beki Mbrazil Milton.Kipindi cha pili timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kunako dakika ya 72 nahodha ya Madrid Karim Benzema aliiandikia timu yake bao la pili akimalizia krosi ya Dani Carvajal.
Kocha wa Barcelona Xavi alifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Ansu Fati na Pedri yaliyoleta matunda kwani dakika ya 83 kinda Fati aliyerejea uwanjani kutoka majeruhi aliisawazisha matokeo ya mchezo kuwa 2-2 na kupelekea uende dakika 30 za ziada.
Kiungo aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Fede Valverde aliipa Real Madrid bao la ushindi dakika ya 98.Ushindi huo umewapeleka Madrid fainali ya michuano hiyo ya tatu kwa ukubwa nchini Hispania.