Klabu ya Simba sc imefikia makubaliano ya kuachana na mchezaji Pa Omar Jobe baada ya kuhudumu klabuni hapo kwa takribani miezi sita pekee baada ya kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili mwezi januari mwaka huu.
Mshambuliaji huyo mrefu mwenye miaka 25 alijiunga na Simba sc baada ya kumaliza mkataba wake na timu ya Zhenis inayoshiriki Ligi Kuu nchini Kazakhstan huku akitarajiwa kufanya makubwa klabuni hapo lakini bahati mbaya alishindwa kukidhi matarajio ya wengi.
Katika taarifa iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii ya klabu hiyo inaeleza kuwa klabu hiyo imeachana na mchezaji huyo na inamtakia kila la kheri huko aendako.
“Kuelekea msimu mpya wa mashindano 2024/25 tumefanya marekebisho makubwa ya kikosi na malengo yetu ni kurejesha makali tuliyokuwa nayo miaka minne iliyopita”.Ilisema taarifa hiyo na kuendelea kuwa inamtakia kila la kheri mchezaji huyo.
“Simba Sc inamtakia kheri Jobe katika maisha mapya ya soka nje ya Simba na siku zote tutaendelea kuthamini mchango wake ndani ya kikosi chetu.” Imeeleza taarifa ya Simba Sc
Jobe alisajiliwa na klabu ya Simba sc kuboresha kikosi chake katika dirisha la usajili la mwezi Januari akiwa sambamba na mshambuliaji Fredy Michael huku klabu hiyo ikiwatema Jean Baleke na Moses Phiri ambao walikua washambuliaji vinara wa klabu hiyo.