Timu ya Taifa ya Ivory Coast wameibuka mabingwa wa kombe la mataifa ya Afrika baada ya kuifunga Nigeria kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali ambapo takribani nchi zote za Afrika zilikua zinashuhudia michuano hiyo kupitia vyanzo mbalimbali vya habari.
Haikutabiriwa na wengi kuwa wenyeji wataibuka mabingwa kutokana na kuanza kwa kusuasua katika hatua ya makundi lakini walibadilika baada ya kuingia hatua ya mtoano ambapo walizifunga timu ngumu kama Congo Drc na Senegal mpaka kufika hatua ya fainali.
Nigeria ilianza kupata bao dakika ya 38 kwa kichwa likifungwa na nahodha William Trost Ekong bao ambalo lilidumu mpaka wakati wa mapumziko lakini kipindi cha pili Frank Kessie aliunganisha kwa kichwa mpira wa kona na kusawazisha bao hilo huku wengi wakisubiri dakika za nyongeza Sebastian Kohler aliibuka shujaa kwa wenyeji akifunga bao gumu kwa kisigino mbele ya msitu wa mabeki wa Nigeria dakika 9 kabla ya mpira kuisha.
Filimbi ya mwisho ilizua shangwe kwa wenyeji wakiongozwa na rais wa nchi hiyo Alassane Ouattara aliyeambatana na mkewe huku maelfu ya mashabiki sambamba na wakongwe Didier Drogba na Wilfred Bonny wakiongoza shangwe katika usiku huo.
Hili ni taji la tatu kwa wenyeji katika michuano hii wakichukua pia miaka ya 1992 na 2015 huku Nigeria pia wao wakilichukua mara tatu mwaka 1980 kisha 1994 na 2013 pia wakiingia fainali mara nane.