Kuelekea mchezo wa kesho wa Kundi B baina ya Simba sc dhidi ya Wydad Athletecs Club ya nchini Morroco timu hizo mbili zimetambiana kuibuka na ushindi katika mchezo huo utakaofanyika saa nne usiku katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
Kocha wa Simba Sc Abdelhack Benchika yeye amesema kuwa timu hiyo inafungika na hivyo ni suala la washambuliaji wa timu yake kutumia nafasi zitakazopatikana katika mchezo huo.
“Hakuna timu isiyofungika, tuondoe mawazo hasi kichwani kwetu tutaingia uwanjani tukiwa kifua mbele na lengo likiwa ni kushinda. Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipa nguvu timu yao naamini baada ya mechi tutafurahi kwa pamoja,” alisema Benchikha
Pia kocha huyo alithibitisha kukosekana kwa viungo wake wawili Sadio Kanoute na Saido Ntibanzokiza kuelekea katika mchezo huo.
“Kesho nitawakosa viungo wangu, Saido Ntibazonkiza pamoja na Sadio Kanoute ila naamini waliobaki wakijituma na kuwa na shauku basi naamini tutafanya vizuri kwa ajili ya mashabiki wa Simba SC”Alisema kocha huyo wa zamani wa Usm Algers.
Kwa upande wa klabu ya Wydad wenyewe wamesema kuwa hawana wasiwasi na mchezo huo huku wakisisitiza kuwa hawawaogopi mashabiki wa Simba sc pamoja na kuwa watajaa uwanjani.
“Sisi Wydad tuna Mashabiki kila ukanda wa Afrika, Tofauti na ilivyo kwa Simba SC.. tunaweza kucheza mechi Algeria na bado tukapata mashabiki wa kutupa sapoti”Alisema golikipa wa klabu hiyo Youssef El Motie
“Hatujawahi kuogopa mashabiki wa wapinzani wetu na ndio maana msimu huu tumecheza mechi za AFL kule Nigeria na Afrika Kusini na kote tulishangiliwa.”Aliendelea kusema kipa huyo
“Tumekuja kutafuta alama Tatu hapa Tanzania hilo ndio la muhimu na kuhusu wingi wa mashabiki wa simba kuwepo kesho hilo halitoweza kutusumbua kwani hata sisi mashabiki wetu kutoka hapa Tanzania na Morocco watakuwepo kutupa sapoti”.Alimalizia kusema mbele ya waandishi wa habari.
Mpaka sasa katika msimamo wa kundi hilo Asec Mimosa yupo kileleni akiwa na alama 7 huku Jwaneng Galaxy akiwa katika nafasi ya pili ya msimamo na alama 4 na Wydad yupo nafasi ya tatu akiwa na alama tatu na Simba sc akiwa mkiani mwa kundi hilo B na alama 2.