Kufuatia kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Cbe SA ya nchini Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya pili ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika kocha wa klabu ya Yanga sc Miguel Gamondi amegeuka mbogo kwa mastaa wa klabu hiyo kutokana na kukosa mabao ya wazi.
Mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Abebe Bikila nchini humo ilishuhudiwa Yanga sc ikikosa mabao kadhaa ya wazi ambapo Prince Mpumelelo Dube alikosa nafasi tatu za wazi kabla ya kufunga katika nafasi ya nne dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza akipokea pasi ya Pacome Zouzoua.
Kipindi cha pili pamoja na wenyeji kucheza mchezo wa pasi fupi fupi ilishuhudiwa pia mastaa Max Nzengeli na Clement Mzize nao wakikosa mabao ya wazi katika mchezo huo.
“Kiukweli nashindwa kuelewa shida ni nini kwa maana tunatengeneza nafasi nyingi lakini tunashindwa kuzitumia kabisa hali ambayo inanichanganya sana”Alisema kocha Miguel Gamondi wakati walipowasili uwanja wa ndege wa J.K Nyerere akitokea nchini Ethiopia.
Yanga sc itakua na kazi ngumu katika dakika 90 za marejeano na Waethiopia hao mchezo utakaofanyika Septemba 21 visiwani Zanzibar katika uwanja wa Amani ambapo matokeo ya sare ama ushindi wa aina yeyote utaivusha klabu hiyo kwenda katika hatua ya makundi ya kombe la Klabu bingwa barani Afrika kwa mara ya pili mfululizo.