Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF) lipo mbioni kubadili uwanja utakaofanyika mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho la Crdb ambao umepangwa kufanyika mkoani Manyara katika uwanja wa Tanzanite siku ya June 2 mwaka huu.
TFF inafikiria kubadili uwanja kutokana na sababu kubwa tatu ambazo ni uwanja kuwa na uwezo mdogo wa kuingiza mashabiki huku eneo la Babati mkoani Manyara linakabiliwa na upungufu mkubwa wa miundombini kuweza kuwahudumia maelfu ya mashabiki watakaofika mkoani Manyara kuhudhuria mchezo huo.
Sababu nyingine kubwa ya kuhamisha mchezo huo ni sababu za kibiashara zaidi kutokana na ukweli kwamba endapo mchezo huo utafanyika katika miji mikubwa basi hata mdhamini wa michuano hiyo benki ya Crdb sambamba na wadhamini wenza kama vile Azamtv watapata coverage kubwa zaidi kuliko ikifanyika Babati.
Mpaka sasa viwanja vinavyotajwa kuwa mchezo huo unaweza kuhamishiwa huko ni uwanja wa Ccm Kirumba jijini Mwanza,Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam huku uwanja wa Sheikh Amri Abeid nao ukitajwa japo unakosa sifa kutokana na kuwa mdogo huku pia ukitoka kuandaa fainali kama hizo msimu wa 2021/2022.
Kikao cha kamati ya utendaji ya TFF ndio ambacho kitaamua kuhusu suala hilo na kinatarajiwa kufanyika wiki hii jijini Dar es salaam.