Mshambuliaji Prince Dube amerejesha mali zote alizopewa na klabu hiyo ikiwemo gari ya kutembelea pamoja na nyumba baada ya kugoma kuendelea kuichezea klabu hiyo ambapo tayari alishawasilisha barua ya kuvunja mkataba wake wa miaka miwili na nusu uliobaki.
Dube aliingia katika mgogoro wa kimkataba na klabu hiyo aliyoichezea kwa miaka minne kutokana na kuwasilisha barua ya kuondoka klabuni hapo ambapo klabu ilimtaka kufata taratibu za kuvunja mkataba ikiwemo kulipa kiasi cha dola laki tatu za kimarekani ili kuondoka klabuni hapa na kama ikishindikana basi hana budi kuendelea kusalia mitaa ya Chamazi.
Pamoja na jibu hilo staa huyo aliamua kulipa kiasi cha dola laki moja na elfu hamsini alichochukua kama pesa ya kusainia mkataba mpya (Signing on fees) lakini klabu hiyo imeshikilia msimamo kuwa lazima alipe kiasi chote kwa mujibu wa mkataba.

Leo sakata hilo limeingia sehemu nyingine baada ya staa huyo kuamua kuaga rasmi kupitia mtandao wake rasmi wa Instagrama ambapo ameushukuru uongozi wa klabu hiyo,wachezaji na benchi la ufundi aliokua nao kwa kipindi chote cha miaka minne.
“Kwa hisia mchanganyiko ninatangaza kuondoka AzamFc ambapo kwa miaka minne imekua safari nzuri ikiwa na changamoto,ushindi na kumbukumbu nzuri,nawashukuru wote tuliokua pamoja kuanzia kwa uongozi mpaka kwa benchi la ufundi,wachezaji wenzangu na kwa namna ya pekee mashabiki”ilisomeka barua hiyo ya Prince Dube.
Mpaka sasa uongozi wa Azam Fc zaidi ya kuthibitisha kuondoka kwa Dube hawajatoa kauli yeyote kuhusiana na hilo ambapo inabaki kuwachanganya mashabiki kuhusu hatma ya mshambuliaji huyo ambaye timu za Yanga sc na Simba sc zinatamani kuwa naye vikosini mwao.