Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) limetoa uamuzi wa kutobadili uwanja wa mechi kama ilivyoomba timu ya Mc Algers kuekea mchezo wa Kundi wa kombe la Klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Yanga sc.
Awali MC Alger kupitia rais wa klabu hiyo, Mohamed Hakim walipeleka barua CAF kuomba kubadilisha uwanja wa mechi kutoka 5 July 1962 na wakitaka kuutumia Ali la Pointe ambapo Caf wamekataa ombi hilo.
Kutokana na uamuzi huo wa Caf mechi hiyo imepangwa kuchezwa Jumamosi ya Disemba 7 katika Uwanja wa 5 July 1962 uliopo katika Mji wa Algiers ambapo ni karibu zaidi na Uwanja wa Ndege wa Houari Boumediene ambao Yanga itatua leo mchana ikitokea Dar es Salaam, hivyo haitawapa wakati mgumu wa kuanzisha safari nyingine kwenda Douera unapopatikana Uwanja wa Ali la Pointe.
Ombi hilo la MC Alger waliangalia mbali zaidi kwani Uwanja wa Ali la Pointe ndiyo wanautumia zaidi kwa mechi za nyumbani za ligi, hivyo wameuzoea zaidi kulinganisha na 5 July 1962.
Kitendo cha CAF kutokubali ombi la wenyeji wa mchezo huo, ni hatua nzuri ambayo Yanga kwao imekuwa nafuu kwani kama mchezo huo ungepelekwa Ali la Pointe,wawakilishi hao wa Tanzania wangelazimika kufanya safari nyingine ya umbali wa kilomita 17.62 kwa gari hadi kufika Douera kutokea Algiers.