kocha wa makipa wa klabu ya Simba sc Dani Cadena amefunguka mambo mbalimbali ndani ya klabu hiyo yanayopelekea klabu hiyo kutofanya vizuri ndani ya uwanja ambapo imeonekana kuwa klabu hiyo ina shida kubwa ya uongozi kuanzia uongozi wa juu mpaka uongozi wa karibu na benchi la ufundi.
Cadena ambaye mkataba wake unafikia tamati juni 30 mwaka huu huku akiweka sharti la kuona mabadiliko katika uongozi na utawala wa klabu ndio atasaini mkataba mpya kusalia klabuni hapo na kama sivyo basi atatafuta malisho mengine ndani ama nje ya nchi.
“Siku mbili kabla ya mechi (Simba Vs Yanga) hakuna aliyeniuliza kitu lakini kwenye kikao cha mechi Kocha mkuu, Robertinho alisema Aishi Manula yuko tayari kwa kucheza mechi hiyo,Hakuniuliza chochote lakini alifanya maamuzi na nilimuheshimu kocha mkuu, kama angeniuliza ningempa mawazo yangu lakini hakuniuliza nikanyamaza”.
“Najua uwezo wa makipa wangu, kabla ya mechi Kocha mkuu huwa ananiuliza maoni yangu lakini kabla ya kucheza na Yanga Sc hakuniuliza, alitoa amri tu, nikamfuata Manula na kumwambia hatakiwi kucheza kutokana na hali yake kiafya, kilichotokea baada ya mechi matokeo yakawa 5-1.”Alisema Cadena ambaye ni Raia wa Hispania.
Kauli hiyo ya kocha huyo inaonyesha kuwa uongozi wa klabu hiyo inawezekana huwa unaingilia majukumu ya benchi la ufundi hali ambayo wakati mwingine huleta mgawanyiko katika kikosi na kupelekea timu kufanya vibaya uwanjani kiasi cha kukosa mataji kwa msimu wa tatu mfululizo sasa.
Mahojiano baina ya kocha huyo na baadhi ya waandishi wa habari yamezua gumzo hapa nchini kutokana na kuweka wazi madudu ya uongozi ndani ya Simba sc hasa katika kipindi hiki ambapo mabosi wakubwa klabuni hapo wakiongozwa na tajiri Mo Dewji wanajaribu kuweka mambo sawa.