Klabu ya Simba sc imemtambulisha rasmi kocha Abdelhak Benchikha mbele ya waandishi wa habari kama kocha mkuu wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili akichukua nafasi ya Roberto Oliveira “Robertinho” ambaye aliondoka klabuni hapo kwa makubaliano ya pande mbili.
Kocha huyo wa zamani wa Usm Algers ametua klabuni hapo akiwa na wasaidizi wake wawili ambapo watachukua nafasi za kocha msaidizi na kocha wa viungo huku ikisemekana kuwa kocha Selemani Matola atakuwepo kama kocha msaidizi namba mbili na kocha Cadena akirudi katika nafasi yake ya kuwafundisha magolikipa.
Katika utambulisho huo kocha huyo alielezea furaha yake kujiunga na klabu hiyo huku akiomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo “Nina furaha kubwa kuwepo hapa. Tangu nilipoanza kuwasiliana na viongozi nilikuwa na shauku ya kuja. Jambo kubwa ambalo naomba ni mashabiki kutupa ushirikiano na naamini kupitia hilo tutafanikiwa pamoja.”Alisema Benchika.
“Kuna mambo mengi ambayo tayari nayajua na nimekuja na mikakati ambayo taifanyia kazi. Kuhusu wachezaji tajua zaidi nikishaanza kazi, kuhusu mashindano ya ndani na kimataifa yote ni muhimu. Mimi ni mpambanaji na nitapambana hadi tutafika.”Alisema
“Mafanikio yatajengwa na Wanasimba wote hilo ndio muhimu zaidi. Kwa wachezaji sitaangalia majina bali anayefanya vizuri, kiwango cha mchezaji ndio kitafanya nimtumie.”Alimalizia kusema kocha huyo raia wa Algeria
Naye Afisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo Iman Kajula alisema kuwa menejimenti ya klabu hiyo imempa kocha huyo uhuru wote wa kufanya kazi bila kumbana huku akielezea namna walivyopambana kumpata.
“Leo tunatamatisha shauku iliyokuwepo kwa siku kadhaa. Haikuwa jambo rahisi maana lengo letu kama klabu tulitaka mwalimu ambaye atatupeleka mbali. Kumpata mwalimu mzuri ni mchakato mkubwa sana.”Alisema Imani.
“Mwalimu Benchikha atakuwepo kwa mkataba wa misimu miwili. Bodi ya Simba, menejimenti ya Simba imempa mwalimu uhuru wa kufanya kazi. Sisi ni moja ya klabu bora Afrika hatuwezi kufanya kazi kwa kumbana na walimu ambao kocha Benchikha amekuja nao ndio aliochukua nao ubingwa wa Shirikisho Afrika na Super Cup huku Kocha Farid amefanya kazi na Benchikha kwa miaka 30 pamoja na kocha Kamal amefanya nae kazi kwa karibu”.
Simba sc imekua na migongano mingi katika uongozi na wachezaji huku pia timu hiyo uwanjani ikishindwa kuonyesha kiwango bora kiasi cha kufungwa mabao 5-1 na watani wao wa jadi Yanga sc.