Klabu ya Azam Fc imeonyesha nia ya kuinasa saini ya mshambuliaji wa klabu ya Yanga sc Clement Mzize baada ya kutuma ofa ya shilingi milioni mia nne kwa klabu ya Yanga sc ili kumsajili mchezaji huyo aliyesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja klabuni hapo.
Azam Fc inaamini kuwa Mzize ni mbadala sahihi wa mshambuliaji Prince Dube klabuni hapo ambaye ana mgogoro wa kimkataba na klabu hiyo akidai kwamba hakusaini mkataba mpya na klabu hiyo zaidi ya ule wa awali ambao unamalizika Juni 2024.
Klabu ya Yanga sc tayari imepokea ofa hiyo ya Mzize huku pia ikidaiwa ina ofa nyingine kutoka klabu ya Watford inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Uingereza ambayo inamhitaji mwishoni mwa msimu huu huku Yanga sc ikiwa na nia ya kumuongezea mkataba mshambuliaji huyo kwa lengo la kumuuza kwa pesa ndefu hapo baadae.
Suala hilo limezua sintofahamu miongoni mwa mashabiki wa soka nchini ambao baadhi ya mashabiki wa Yanga sc wamekua na wasiwasi wa kumkosa mshambuliaji huyo kama walivyomkosa Feisal Salum ikizingatiwa kuwa mchezaji huyo anasimamiwa na Jasmine AbdulRazack ambaye pia anamsimamia Feisal Salum aliyetimkia Azam Fc.
Taarifa za ndani zaidi zinadai kuwa tayari Yanga sc walishakubaliana na mchezaji huyo kuhusu kuongeza mkataba mpya klabuni hapo na tayari alishaingiziwa kiasi cha pesa kama walivyokubaliana ili asalie klabuni hapo.