Baadhi ya mastaa wa klabu ya Yanga sc waliokua majeruhi wamerejea klabuni hapo kutoka katika majeraha huku tayari baadhi yao wakiwa wameungana na kikosi hicho katika mazoezi kujiandaa na mchezo huo ambao utafanyika siku ya Jumamosi machi 30 saa tatu usiku katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
Wachezaji hao ambao walikua majeruhi ni pamoja na Khalid Aucho ambaye anatarajiwa kuungana na timu mazoezini jioni ya leo huku Kibwana Shomari na Zawadi Mauya akiwa tayari wameshajiunga na kikosi cha timu hiyo katika mazoezi yanayoendelea katika viwanja vya Avic Town na Pacome Zouzou ambaye ameonekana jana akiwa na kikosi cha Ivory Coast akiwa benchi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin uliomalizika kwa sare ya 2-2.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema hivi leo Meneja wa Idara ya Habari ya klabu hiyo Ally Kamwe alisema kuwa tayari mastaa hao wameanza mazoezi isipokua Yao Kouasi ambaye mpaka sasa hali yake bado ni asilimia hamsini kushiriki mchezo huo ambapo tayari ameshakabidhiwa kwa daktari wa klabu hiyo kuhakikisha anakua sawa.
“Zawadi Mauya yupo tayari kufanya kazi kubwa dhidi ya Mamelodi Sundowns, Kibwana Shomari anaendelea vizuri, Yao bado ni 50/50 alichanika nyama za paja, Pacome alikuwepo kwenye kikosi cha Ivory Coast dhidi ya Benin na yupo fit kwa zaidi ya 80% na Aucho anaendelea kujifua kujipanga dhidi ya Mamelodi Sundowns.”