Naibu waziri wa habari sanaaa utamaduni na michezo Mh. Hamis Mwinjuma amewaagiza viongozi wa kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBRC) kumuitwa bondia Kennedy Ayo aliyedai kutelekezwa Nchini Tunisia na promota wake ili kumhoji kuhusu suala hilo.
Naibu waziri ametoa maagizo hayo huku akiamini kuwa Serikali ilichafuliwa kwa kuwa haikuhusika na safari yake hivyo anapaswa kueleza Watanzania kilichosababisha akashindwa kusafiri kwa wakati.

“Bondia akitaka kusafiri nje kwenda kucheza pambano na akafika uwanja wa Ndege akawa amekosa kibali, asipewe kibali arudishwe afuate utaratibu wa kupata kibali na utaratibu wa mabondia kutosafiri kwa kibali maalumu umekufa kuanzia leo lakini pia hatuwezi kuruhusu kuendelea kwa mapambano ya holelaholela hivyo anayetaka kuandaa pambano anatakiwa akasajilie BMT”,Alisema Naibu Waziri huyo kipenzi cha Vijana nchini.
“Mapromota hakikisheni kabla hamjaingia mkataba na bondia, unatakiwa kuleta ripoti za Afya ili kujiridhisha hali ya Afya ya Bondia, hatuwezi kuona mabondia wanakufa ulingoni kisa hali ya Afya na hilo ni agizo kwa TPBRC na Baraza la Michezo”,Aliendelea kusema.
“Kuhusu bima binafsi nitafanya majadiliano na baadhi ya wadau wa bima ili mabondia waweze kupata bima walau hata za muda mfupi zitakazowasaidia katika kipindi kifupi wanachotaka kupanda ulingoni ili kuwalinda mabondia”,Alimalizia kusema hayo huku wadau wa ngumi nchini wakimsikiliza kwa umakini mkubwa.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamisi Mwijuma (Mwana FA) amezungumza na Wadau wa Mchezo wa ngumi Nchini kutokana na kuongezeka kwa matukio yaliyozua taharuki kwa jamii kwa siku za hivi karibuni.