Bondia wa Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania Mohamedi Mnemwa amelazimika kupewa rufaa ya kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwenye kitengo cha Mifupa (Moi) kufuatia kipimo cha CT Scan kuonyesha damu imevilia kwenye ubongo.
Bondia huyo alipata tatizo hilo baada ya kupigwa kwa mapema raundi ya tatu na bondia Ally Msewe siku ya Januari 24 lakini baada ya kupita siku kadhaa tatizo hilo limejulikana kutokana na hali ya bondia huyo kutokua nzuri.
Tatizo hilo liligundulika mchana wa Jumatatu Januari 27, 2024 baada ya kufanyiwa kipimo katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke hali iliyolazimu kuandikiwa rufaa ya kupelekwa Muhimbili.
Katika pambano la raundi nne dhidi ya Ally Issa Sewe lililofanyika Ukumbi wa Mrina uliopo TipTop, Manzese jijini Dar es Salaam bondia huyo alipoteza pambano hilo lenye raundi nne katika raundi ya tatu kwa kupigwa ngumi nzito na kuzimia hali iliyomlazimu mwamuzi kumaliza pambano hilo (Technical Knockout).
Daktari wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Dkt. Hadija Hamisi amesema kuwa hali hiyo ilijulikana baada ya kufanya vipimo vya CTScan.
“Mgonjwa ameshafanyiwa kipimo cha CT Scan na amegundulika kuwa damu imevilia kwenye ubongo, anapelekwa Moi Muhimbili kwa ajili ya kupata vipimo zaidi na tunatarajia watatupa majibu zaidi”,Alisema daktari huyo.
Naibu Waziri wa habari sanaaa na michezo Hamisi Mwijuma tayari alishatoa maelekezo kwa bodi ya Ngumi za Kulipwa Tanzania kuhakikisha mabondia nchini wanakua na bima ili kupata matibabu mazuri pindi wanapoumia.