Connect with us

Makala

Yanga Sc Yawasili Mbarali Kulipa Kisasi

Kikosi cha klabu ya Yanga sc kimefanikiwa kuwasili mkoani Mbeya na kupitiliza kwenda Mbarali tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ihefu Fc utakaofanyika siku ya kesho katika uwanja wa Highland Estates ulioko eneo hilo.

Yanga sc imewasili ikiwa na kumbukumbu ya kupigwa 2-1 msimu uliopita uwanjani hapo na kushindwa kuifikia rekodi ya kutofungwa mechi 50 kama walivyokua wamejipangia ili kuweka rekodi katika uga wa soka barani Afrika.

Kikosi hicho pamoja na kuwasili pia kocha Miguel Gamondi ameelezea hali ya kikosi hicho huku akilalamika ugumu wa ratiba hasa kusafiri umbali mrefu na kikosi ambapo baada ya mchezo huo watapaswa kwenda Mwanza kuwavaa Geita Gold Sc.

“Tunafahamu kwamba ni mwanzo wa ligi na kila timu iko kwenye nafasi nzuri na kujaribu kufanya vizuri zaidi inapokutana na bingwa mtetezi, ni sisi sasa kuhakikisha tunaendelea kucheza kwa kiwango cha juu na nina imani tutaendelea kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na kufanya vizuri kwenye mchezo wa kesho” Alisema kocha Gamondi

“Tunashukuru tumefika salama Mbeya, hatukuweza kupata muda mzuri wa kujiandaa kama mnavyojua tumetoka kucheza mchezo wa Kimataifa Jumamosi lakini tunajua umuhimu wa mchezo wa kesho dhidi ya Ihefu na tutafanya kila jitihada kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye mchezo huu” Miguel Gamondi

Naye kiungo Mudathiri Yahaya akizungumza kwa niaba ya wachezaji wa klabu hiyo alisema “Kwa niaba ya wachezaji wenzangu napenda kuchukua fursa hii kwanza kumshukuru mwenyezi Mungu tumefika salama na tumekuja hapa kupambana na kuhakikisha tunaondoka na alama tatu kwenye mchezo wetu wa kesho”.

Yanga sc tayari ipo kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Nbc ikiwa na alama tisa huku Ihefu Fc ikiwa katika nafasi ya kumi na moja ikiwa na alama tatu.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala