Connect with us

Makala

Yanga sc Yavunja Mwiko Nigeria

Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika uliofanyika katika uwanja wa Godswill Akpabio nchini Nigeria.

Yanga sc ilianza mchezo kwa kuwaheshimu Rivers United kwa kutumia mfumo wa 3-5-2 uliowaruhusu kushambulia na kuzuia kwa nguvu huku wakiwa na idadi kubwa ya walinzi pindi wakishambuliwa ambapo Djuma Shabani,Joyce Lomalisa,Dickson Job,Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad Bacca wakihusika zaidi katika majukumu hayo.

Rivers United wao walianza mchezo kwa kushambulia mwanzoni huku wakipitisha mashambulizi yao eneo la katikati mwa uwanja lakini uimara wa walinzi wa Yanga sc ulifanikisha kuzima mashambulizi hayo bila kuleta madhara ambapo mara nyingi walipokonywa mpira na Yanga sc kushambulia kwa kushtukiza huku Stephane Aziz Ki akikosa mabao mawili ya wazi kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kocha Nasreddine Nabi alibadili mbinu na kuamua kushambulia akiwaingiza Tuisila Kisinda,Jesus Moloko na Kibwana Shomari kuchukua nafasi ya Farid Musa,Joyce Lomalisa hali ambayo iliwaruhusu Yanga sc kushambulia kwa kasi zaidi na hatimaye kupata bao la kwanza dakika ya 73 likifungwa na Fiston Mayele aliyepokea pasi safi ya Bakari Mwamnyeto.

Rivers United baada ya bao hilo waliamua kushambulia bila kuchukua tahadhari ambapo mpira wa faulo walioupiga uliwahiwa na wachezaji wa Yanga sc ambapo Jesus Moloko alikimbia takribani mita 30 na kutoa pasi kwa Mayele aliyempasia Mwamnyeto kisha naye akampasia Mayele na kufunga bao la pili kwa Yanga sc dakika ya 81 ambapo mpaka dakika 90 zinakamilika Yanga sc ilimaliza kwa ushindi huo ugenini.

Sasa Yanga sc wanarejea nchini kuwasubiri Rivers United katika mchezo wa marudio utakaofanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa wikiendi ijayo.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala