Klabu ya Yanga sc imeshindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya kombe la Mapinduzi Cup baada ya kutoka sare ya 1-1 na Singida Big Stars katika mchezo wa mwisho wa kundi B ambalo lilikua na timu za Yanga sc,Singida Big Stars na KmKm ya Zanzibar.
Licha ya kuibuka na ushindi dhidi ya Kmkm iliwapasa Yanga sc washinde mchezo dhidi ya Singida Big Stars inayonolewa na kocha wa zamani wa klabu hiyo Hans Van Pluijm lakini matokeo hayo ya sare yameifanya Singida Big Stars kufuzu nusu fainali kwa faida ya kuwa na wastani wa magoli mengi na kuwazidi Yanga sc.
Singida Big Stars waliingiza kikosi kamili katika mchezo huo kama ambavyo hufanya katika michezo ya ligi kuu ambapo mastaa kama Said Ndemla,Bruno Gomez,Deus Kaseke,Nickson Kibabage wakichanganya na wachezaji wapya kama Fancy Kazadi na Yusuph Kagoma ambapo walifanikiwa kupata bao dakika ya 22 likifungwa na Kazadi baada ya kipa wa Yanga sc kutema mpira.
Faulo ya David Bryson iliwasawazishia Yanga sc bao hilo dakika ya 31 na licha ya mashambulizi makali langoni mwa wapinzani wao kutokua makini kwa Dickson Ambundo na Clement Mzize pamoja na Yacouba Songne kuliwanyima mabao kadhaa huku Lazarus Kambole akishindwa kabisa kuonyesha cheche baada ya kuingia mwishoni mwa kipindi cha pili na kufanya mpira kumalizika kwa 1-1.