Baada ya kuibamiza Azam Fc kwa bao 1-0 klabu ya Yanga sc imefanikiwa kubeba mataji yote nchini kwa msimu wa 2022/2023 yakiwemo ya Ligi kuu ya Nbc,Ngao ya hisani na kombe la shirikisho la Azam ambalo wameshinda jioni ya leo.
Yanga sc iliingia katika fainali hizo baada ya kuitoa Singida Big Stars kwa bao 1-0 lililofungwa na Fiston Kalala Mayele na leo wameweza kuifunga Azam Fc katika fainali hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Yanga sc ikiingia uwanjani bila mastaa Fiston Mayele,Aziz Ki na Jesus Moloko ilifanikiwa kupata bao la mapema kupitia kwa Kennedy Musonda dakika ya 13 ya mchezo aliyepata krosi kutoka kwa Tuisila Kisinda na kufunga kwa kichwa na kuwaacha mabeki wa Azam Fc wakiwa hawana la kufanya.
Katika kipindi cha kwanza Yanga sc walijenga mashambulizi kwa ustadi mkubwa huku wakikosa nafasi kadhaa na kuwashangaza wengi walivyozima makali ya Azam Fc ambao waliamka kipindi cha pili hasa baada ya kuingia Prince Dube na Kipre Jr ambao walikua na kasi ya kushambulia huku Abdul Sopu akikosa nafasi kadhaa za wazi.
Yanga sc kipindi cha pili ilipoozesha mchezo mara kadhaa ili kupunguza kasi ya Azam Fc na mpaka mpira unaisha matokeo yalibaki bao moja kwa Yanga sc na kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo kuhitimisha msimu kwa furaha iliyoje baada ya kutwaa mataji yote matatu.