Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa stars) kimefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika 2025 dhidi ya Guinea uliofanyika ugenini Guinea.
Stars iliingia mchezoni ikiwa na kumbukumbu ya suluhu dhidi ya Ethiopia katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kuwaibua mashabiki na wadau wa soka kutokana na kiwango kilichozua tafrani na kuwafanya kuanza kuwakumbuka mastaa Mbwana Samata na Simon Msuva ambao wamepumzika kuitumikia timu hiyo.
Guinea ilifanya mashambulizi makali langoni mwa stars lakini mpaka mapumziko matokeo yalisalia suluhu huku kipindi cha pili dakika ya 58 makosa ya safu ya kiungo ya Stars yaliipa Guinea uongozi licha ya jitihada za Ibrahim Hamad Bacca kuokoa mpira huo uliopigwa na Mohammed Camara.
Dakika ya 68 Feisal Salum alipokea pasi safi akiwa mbali na lango la wapinzani na kupiga shuti kali lililozama moja kwa moja wavuni.
Wakati Guinea wakijiuliza kuhusu bao hilo na kuamua kushambulia kwa kasi na kujikuta wanafungwa bao la pili dakika ya 88 na Mudathir Yahaya aliyemalizia mpira uliotemwa na kipa wa timu hiyo akiokoa shuti kali la Feisal Salum.
Dakika 90 zilimalizika kwa Stars kuchukua alama tatu na kukaa katika nafasi ya pili ya kundi H wakiwa na alama 4 huku Congo Drc wakiwa kileleni na alama 6 na Ethiopia ikiwa nafasi ya tatu na alama 1 na Guinea wakiwa hawana alama na timu zote zikiwa zimecheza michezo miwili.