Connect with us

Makala

Simba Sc Week Kuanzia Mikumi

Klabu ya Simba sc imetangaza kuwa wiki maalumu ya klabu hiyo kuelekea tamasha la Simba Sc Day inatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 24 katika mbuga ya Wanyama ya Mikumi mkoani Morogoro ambapo kutakua na shughli mbalimbali za utalii ikiwemo mashabiki kupata fursa ya kupanda treni ya mwendokasi ya Sgr.

Hayo yametangazwa katika mkutano maalumu na Waandishi wa habari uliofanyika katika kituo cha Treni hiyo ya mwendokasi kilichopo katikati ya Jiji la Dar es salaam ambapo pia mbali na Menejimenti ya reli ya mwendokasi kushiriki pia Bodi ya utalii nao walikuwepo katika Mkutano huo.

“Lengo la mkutano huu ni kutangaza rasmi kuanza kwa Wiki ya Simba 2024 pamoja na maandalizi yote kuelekea Siku ya Simba (Simba Day). Kama mnavyojua kila mwaka tunajaribu kufanya jambo jipya ili kuongeza thamani ya jambo letu.”Alisema Meneja wa Idara ya Habari ya klabu ya Simba Sc.

“Twendeni Hifadhi ya Mikumi tukawaonyeshe Watanznia kuna hifadhi, ni karibu na kiingilio ni 5,900. Kuna wengine wakisikia utalii wanajua ni mamilioni kumbe ni hela kidogo. Lakini pia ni kwenda kutangaza treni mpya ya SGR. Kwanza ni bidhaa mpya ambayo inatakiwa kutangazwa na sisi Simba Sports Club ndio Wenye Nchi kuitangaza.”Aliendelea kusema Ahmed ambaye alipata umaarufu zaidi alipokua akitangaza katika kituo cha Azamtv

Naye Mtendaji mkuu wa klabu hiyo Iman Kajula alitanabaisha ya kuwa katika wiki hiyo kutakua na matukio mbalimbali ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu ambao utafanyika katika mbuga hiyo ya mikumi.

“Kwenye mbuga ya Mikumi sio tu kufanya uzinduzi na kurudi, kuna uwanja mzuri sana wa mpura na Ahmed atazungusha namba 6, yawezekana pia Ally Kiba akawepo. Mimi tazungusha namba 10. Ubaya Ubwela hadi kwenye mbuga za wanyama.”Alisema Kajula ambaye anatarajiwa kuondoka katika nafasi hiyo ifikapo mwishoni mwa mwezi wa nane mwaka huu.

Kwa upande wa Mhifadhi mkuu wa Mbuga ya Mikumi  Agustino Masesa yeye alisema kuwa wako tayari kupokea ugeni huo sambamba na kuwatembeza katika maeneo tofauti tofauti ya hifadhi ili waweze kujionea mambo mbalimbali ya utalii.

“Simba inakuja Mikumi na Mikumi kuna Simba. Mnakuja kukutana na Simba wa kweli. Tunawakaribisha sana na tunawashukuru sana kwa kutupa heshima ya kuja kuzindulia Simba Week kwenye hifadhi yetu.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa yeye alisema kwamba anashukuru kwa klabu hiyo kuamua kuwashirikisha jambo hilo huku akisisitiza kuwa wapo tayari kuwahudumia mashabiki watakaojitokeza kwa nauli ya shilingi 13000/= tu.

“Tunawashukuru Simba kwa kutushirikisha kwenye tukio kama hili, biashara yetu ni kusafirisha watu na mizigo. Tukio kama hili linatupa faida kubwa kibiashara maana tukio kama hili litaangaliwa na mamilioni ya watu. Lina faida kubwa pia kwa serikali kwa wananchi kuona serikali yao inafanya nini.” Alisema Kadogosa

“Tutashirikiana na ninyi kwa kwenda na kurudi pamoja Morogoro na hata ukiangalia nauli zetu ni rafiki Tsh. 13,000 tu. Tunawashukuru sana kwa tukio hili, ni tukio la kizalendo, kwa sisi SGR ni jambo kubwa tunahitaji kuonekana.”Alimalizia kusema

Kwa upande wa bodi ya utalii nchini ambayo iliwakilishwa na Afisa Masoko Nassor Garamatatu alielezea sababu iliyoifanya bodi hiyo kuamua kushirikiana na klabu ya Simba sc katika tukio hilo lenye mvuto kwa mashabiki.

“Tumeingia ushirikiano huu kwa sababu kuu mbili, moja kuhamasisha utalii wa ndani na nje kupitia uzinduzi wa Wiki ya Simba. Sababu namba mbili tunafahamu ushawishi Klabu ya Simba imekuwa nao kwenye mitandao ya kijamii. Wamefanya kampeni nyingi za aina hii kama ya mwaka jana kwenda Mlima Kilimanjaro na Visit Zanzibar hivyo tunaamini kampeni hii itatoa hamasa kwa Watanzania kwenda kwenye vivutio vilivyo karibu nao kwa kutumia treni ya SGR.”Alisema

Simba week limekua ni tukio kubwa hasa siku ya kilele chake yaani Simba Day ambapo maelfu ya mashabiki hukusanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa kuangalia utambulisho wa mastaa wapya klabuni hapo.

 

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala