Kikosi cha Simba sc kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Wydad Ac mchezo utakaofanyika usiku wa leo saa nne usiku ikiwa ni saa mbili usiku kwa saa za nchini Morocco huku mchezo ukifanyika katika uwanja wa Mohamed.
Simba sc iliwasili nchini humo katikati ya wiki hii kwa makundi mawili kutokana na changamoto ya usafiri kufika nchini humo na tayari kwa mujibu wa benchi la ufundi la timu hiyo kikosi kipo imara huku kukiwa na majeruhi kadhaa waliobaki nchini akiwemo kipa Aishi Manula.
“Itakua ni mechi ya tofauti sababu tunacheza nje ya Tanzania na tumejalibu mbinu mbili kwenye wiki hii na leo na kesho{leo} kwa kushirikiana na wenzangu tutaamua mbinu ya kutumia kwenye mchezo huu,Naamini katika vipaji walivyonavyo wachezaji wetu” Alisema kocha wa klabu hiyo Mbrazil Robertinho.
Kwa upande wa mastaa wa klabu hiyo walioko nchini Morocco wamesema wako tayari kwa mchezo huo na wanasubiri muda ufike warejeshe furaha nchini.
“Tuko tayari kupambana,Tumejituma sana hadi kufikia hatua hii hivyo tutaendelea kupambana ili tufuzu nusu fainali”Alisema Pape Osmane Sakho winga wa klabu hiyo.
Simba sc inahitaji ushindi katika mchezo huo ama sare ya aina yeyote ili ifuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za vilabu barani Afrika hatua ambayo hawajafikia kwa miaka ya hivi karibuni.