Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema mabadiliko, jitihada na mipango mbalimbali inayoendelea kufanywa ndani ya timu ya Pamba Jiji FC kuhakikisha inarejesha makali yake na kupanda kwenda Ligi Kuu, siyo ya kubahatisha kwani wamedhamiria kweli kweli na hakuna wa kuwaangusha.
Makalla ambaye ni mlezi wa Pamba Jiji FC ambayo kwa sasa iko chini ya umiliki na uendeshaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, ametoa kauli hiyo leo Agosti 18, 2023 wakati akizungumza na wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo katika Uwanja wa Nyamagana jijini hapa.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwapa wachezaji motisha ya Sh1 milioni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano ambaye pia amekabidhi Sh1 milioni kwa wachezaji wa timu hiyo.
Kocha wa Pamba Jiji FC, Mbwana Makatta, amesema amekuwa na kikosi hicho kwa wiki mbili akifanya mchujo wa wachezaji 100 na sasa amebakiza takribani 30 ambao watapunguzwa tena, huku akiahidi kuwa anatengeneza timu ya ushindani itakayompa matokeo kwani ana wachezaji wengi wazoefu kutoka Ligi Kuu.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano, amewataka wachezaji wa timu hiyo kuondoa shaka kwani chama hicho kitashirikiana nao muda wote pamoja na ofisi ya halmashauri ili wapate wanachostahili ikiwamo mazingira mazuri ya kazi na motisha.
Credit:VanforSports