Klabu ya Juventus imesema itavunja mkataba na nyota wake raia wa Ufaransa Paul Pogba kama atafungiwa kujihusisha na soka kutokana na tuhuma zake za kutumia dawa za kusisimua misuli ambazo zinapigwa vita michezoni.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United ameandamwa na mikosi mingi ikiwemo hali ya kuwa majeruhi mara kwa mara huku pia akiwa amegombana na kaka zake Mathias na rafiki zake kwa tuhuma za kutaka kumuibia kiasi cha Paundi milioni 11 ambapo sasa kesi ipo mahakamani.
Janga jingine jipya linamuandama staa huyo ambapo anachunguzwa na mahakama ya kitaifa ya kupambana na utumiaji wa madawa ya kulevya nchini Italia baada ya kukutwa na kiwango kikubwa cha homoni za Testosteroni ambazo husababishwa na kutumia dawa za kusisimua misuli kwa kiwango kikubwa.
August 20 katika mchezo wa ligi kuu ya nchini humo (Serie A) dhidi ya Udinese mamlaka hiyo ilifanya vipimo kwa wachezaji ambapo staa huyo aligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha homoni hizo na hivyo sasa amesimamishwa kwa muda kupisha uchunguzi.
Endapo staa huyo atabainika alitumia dawa hizo basi anaweza kufungiwa kwa miaka kati ya miwili mpaka minne huku tayari klabu yake ya Juventus ikifuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi.
“Klabu ya Juventus inatangaza kwamba leo Septemba 11 mchezaji Paulo Pogba amepokea kifungo cha muda kutoka kwa mahakama ya kitaifa ya kupambana na utumiaji wa madawa ya kulevya baada ya kukutwa na majibu chanya katika vipimo vya August 20 hivyo klabu inafuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi ili kuchukua hatua”ilisomeka taarifa kutoka klabuni humo.