Kipa wa klabu ya Yanga sc Metacha Mnata amesimamishwa kwa muda na kocha Miguel Gamondi baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu kwa mara ya pili akichelewa kuripoti kambini kutoka katika majukumu ya timu ya Taifa tofauti na wenzake ambao walifika kwa muda uliopangwa.
Kocha Gamondi amefikia hatua hiyo baada ya siku chache zilizopita kumfungia staa huyo kushiriki mazoezi na timu hiyo sambamba na Jonas Mkude baada ya kuchelewa kujiunga na kambi ya timu hiyo iliyokua ikijiandaa na mchezo dhidi ya Ihefu Fc.
Baada ya kurejea na kusamehewa kosa hilo kipa huyo tena amerudia tabia hiyo baada ya kuitwa timu ya taifa kujiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Sudan uliofanyika nchini falme za kiarabu ambapo stars ilitoka 1-1 ambapo baada ya kurejea nchini mastaa walipaswa kuwahi kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam Fc.
“Alipowatafuta viongozi ili arudi, tumeambiwa kocha (Miguel Gamondi), alizuia asirejee kwanza akichukizwa na kitu alichokifanya cha kukaa kimya huku wengine waliokuwa naye kwenye timu hiyo ya taifa wakiwa wamerudi,” amesema mmoja wa viongozi wa timu hiyo.
“Hatujajua amechukuliwa hatua gani, lakini kwenye timu ilikuwa bado hajarudishwa nadhani kuna mawasiliano anayafanya na viongozi kwanza.”Kilisema chanzo kutoka klabuni humo
Tangu anasajiliwa klabuni hapo kwa mara ya pili akitokea Singida Fountain Gate Fc mashabiki wa Yanga sc walionyesha wasiwasi hasa kuhusu nidhamu ya kipa huyo ambaye aliondoka klabuni hapo kutokana na kuwatusi mashabiki wa klabu hiyo kwa ishara katika uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo dhidi ya Mwadui Fc.