Kikosi cha jumla ya mastaa 25 pamoja na viongozi wakiwemo wa benchi la ufundi tisa watapaa jioni ya leo kuelekea nchini Tunisia kwenda kuwavaa Us Monastry katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika utakaofanyika siku ya Jumapili nchini humo.
Yanga sc imesafiri takribani na mastaa wake wote wa kikosi cha kwanza akiwemo kipa AbouTwilib Mshery ambaye anakwenda kwa ajili ya matibabu huku mawinga Dennis Nkane na Benard Morrison wakikosekana kutokana na kuwa na majeraha ya muda mrefu kiasi.
Katika safari hiyo Yanga sc inatarajiwa kupitia Dubai kwa ajili ya mapumziko mafupi “Tunaondoka Dar Es Salaam leo saa 9:25 alasiri kuelekea Dubai, ambapo tutapumzika hapo na kesho tutaondoka kuelekea Tunisia, tunasafiri na wachezaji 25 na benchi la ufundi 9 pamoja na Aboutwalib Mshery akienda kwa ajili ya matibabu na Mwalimu Nabi akiwa ameshatangulia Tunisia kwa ajili ya maandalizi” Afisa habari Young Africans SC Ally Kamwe.
Bahati nzuri kwa Yanga sc inakwenda kucheza katika taifa ambalo wana ufahamu na wenyeji wa kutosha wa nchi hiyo ambapo ni nyumbani kwa kocha mkuu Nasredine Nabi huku mchezo utachezwa katika uwanja wa Stade Olympique Hamadi Agrebi ambao walicheza na kuwafunga Club Africain katika hatua ya mtoano wa michuano hiyo.