Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuibuka mabingwa wa kombe la Shirikisho la Crdb baada ya kuifunga Azam Fc kwa mikwaju ya penati 6-5 baada ya kila timu kupiga penati 9 kutokana na kutopatikana kwa mshindi katika dakika 90 na 30 za nyongeza.
Kocha Miguel Gamond aliamua kumuanzisha Pacome Zouzou,Maxi Nzengeli sambamba na Stephane Aziz Ki pamoja na pacha ya Mudathir Yahya na Khalid Aucho ambao waliwapa tabu viungo wa Azam Fc Yahaya Zayd na Adolph Bitegeko ambao walizidiwa maarifa licha ya kuwa na mawinga bora zaidi mchezoni wakiongozwa na Gibril Sillah na Kipre Junior.
Azam Fc wamshukuru kipa Mohamed Mustapha kwa kuwaweka mchezoni mara kwa mara akipangua mipira kadhaa ya Aziz Ki,Mudathir Yahya na Clement Mzize huku Djigui Diarra yeye hakupata kashikashi kubwa sana kutokana na ukuta wake ulikua upo mchezoni mara kwa mara.
Ahmed Arajiga alimaliza dakika 90 za mchezo na kuongeza dakika 30 ambazo zilitawaliwa na kosa kosa za kila upande huku beki Dickson Job akibahatika kumaliza dakika hizo salama kutokana na kucheza akiwa na kadi ya njano na alishaonywa zaidi ya mara moja na mwamuzi sababu ya faulo.
Kipa Mohamed Mustapha alifanya kazi ya ziada kuoka penati za Joseph Guede na Stephane Aziz Ki lakini uimara wa kipa Djigui Diara ambaye aliokoa penati ya Lusajo Mwaikenda na kuwaweka mchezoni na baada ya piga nikupige Idd Nado alikosa penati na kuipa Yanga sc ubingwa wa tatu mfululizo wa michuano hiyo.
Sasa Yanga sc msimu huu imebeba mataji makubwa wa ligi kuu na kombe la shirikisho kwa mara ya tatu mfululizo huku ikikosa ngao ya jamii ambayo imeenda kwa Simba sc na pia mfungaji bora ni Clement Mzize mwenye mabao matano katika michuano hiyo.