Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) limesogeza mbele michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) iliyokua inatarajiwa ianze kutimua vumbi kuanzia 01 Februari 2025 hadi 28 Februari 2025 katika nchi za Tanzania,Kenya na Uganda.
Kutokana na uamuzi huo sasa michuano hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia mwezi August mwaka huu katika nchi hizo hizo.
Uamuzi huo umekuja kutokana na ushauri walioutoa wataalamu wa Kiufundi wanaohusika na masuala ya Miundombinu kutoka CAF, ambao baadhi yao wakiwa wameweka kambi nchini Kenya, Tanzania, na Uganda, wameishauri CAF kuwa muda zaidi unahitajika ili kuhakikisha kuwa miundombinu na vifaa viko katika viwango vinavyohitajika kwa ajili ya kuandaa mashindano hayo ya Mataifa ya Afrika.
Taarifa rasmi ya kusimamishwa kwa michuano hiyo imetolewa na Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe.
“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Rais William Ruto wa Kenya, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa uongozi wao, kujitolea kwao, na maendeleo mazuri yaliyopatikana katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo, viwanja vya mazoezi, hoteli, hospitali, na miundombinu mingine nchini Kenya, Tanzania, na Uganda kwa ajili ya kuandaa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (CHAN)2024”,Alisema Dr.Motsepe
“Nimevutiwa na ujenzi unaoendelea na ukarabati wa miundombinu ya soka na vifaa katika nchi za Kenya, Tanzania, na Uganda. Nina imani kuwa viwanja vya michezo, viwanja vya mazoezi, hoteli, hospitali, na miundombinu mingine vitakuwa katika viwango vinavyotakiwa na CAF kwa ajili ya kuandaa Mashindano hayo ifikapo mwezi Agosti 2025”,Aliendelea kusema Dk.Motsepe ambaye ni Rais wa Shirikisho hilo.
Tarehe halisi ya kuanza kwa Mashindano hayo itatangazwa kabla ya mwezi Agosti 2025 na CAF hapo baadae baada ya kumaliza maandalizi na taratibu zote za ndani.