Baada ya Simba sc kuthibitisha kumuongezea mkataba mshambuliaji John Boko wa miaka miwili utata umezuka baada ya taarifa kusambaa kuwa mchezaji huyo pia alisaini mkataba wa awali na Polokwane City ya Afrika kusini mkataba ambao inasemekana alisaini baada ya mechi ya Tp Mazembe iliyofanyika Dar es salaam.
Mkataba huo wa awali unaonyesha ungeanza rasmi julai mosi 2019 hadi juni 31, 2021 hivyo mchezaji huyo alikua anasubiri mkataba wake kuisha rasmi ili kutangazwa na klabu hiyo inayocheza ligi kuu Afrika kusini.
Kwa mujibu wa kanuni za usajili za Fifa mchezaji huyo endapo itathibitika amesaini timu mbili ataingia matatani kwani ni kinyume cha kanuni japo Polokwane walikua wanaruhusiwa kuzungumza na mchezaji huyo kwani mkataba wake ulikua chini ya miezi sita kama kanuni inavyosema bali kitendo cha mchezaji huyo kusaini timu zote ndicho kitakachomuweka matatani.
Kwa mujibu wa Simba sc kupitia mtendaji mkuu wa klabu hiyo Crescentius Magori alisema kuwa Polokwane hawakufata taratibu za usajili kwa kuzungumza na mchezaji huyo bila kuwashirikisha Simba sc kitu ambacho baadhi ya wadau wa soka wamekitilia shaka kwani mchezaji akiwa na mkataba chini ya miezi sita anaruhusiwa kuzungumza na timu yeyote kuhusu mkataba mpya.
Endapo timu hizo mbili hazitofikia muafaka na kuamua kulipeleka suala hilo Fifa mchezaji huyo mrefu mwenye mabao zaidi ya 30 aliyoifungia Simba toka ajiunge nao miaka miwili iliyopita anaweza kupata adhabu ya kufungiwa ama kupigwa faini.