Ndio msemo uliotawala midomoni mwa mashabiki wa klabu za Simba sc na Yanga sc baada ya dakika tisini za mechi ya ligi kuu nchini uliofanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam na kumalizika kwa sare ya 1-1.
Simba sc iliyoanza na safu ya ushambuliaji chini ya Moses Phiri akisaidiwa na Cletous Chama na mawinga Augustine Okrah na Pape Osmane Sakho ilipata bao la mapema dakika ya 15 ya mchezo baada ya Chama kumpa pasi Okrah aliyekua amewatoroka mabeki wa Yanga sc na kumchungulia kipa Djigui Diarra na kuandika bao hilo lililoamsha shangwe kwa mashabiki wa Simba sc waliofurika uwanjani hapo.
Yanga sc iliyoanza na Fiston Mayele akisaidiwa na Stephane Aziz Ki pamoja na mawinga Jesus Moloko na Tuisila Kisinda walifanya mashambulizi mengi ambayo yalishindwa kuzaa bao kutokana na kukosekana kwa utulivu hasa kwa Kisinda ambaye mara nyingi hakua na mipira sahihi ya mwisho.
Stephane Azizi Ki alidhihirisha ubora wake baada ya kufunga kwa faulo dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza ambapo alipiga shuti kali lililomshinda Kipa Aishi Manula na kujaa wavuni na kufanya dakika 45 za kwanza kukamilika kwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili kila timu ilijitahidi kutafuta bao huku zikifanya mabadiliko kadhaa ili kuongeza ufanisi ambapo Yanga sc ilimuingiza Farid Musa na Gael Bigirimana katika nafasi ya Tuisila Kisinda na Jesus Moloko huku Simba sc ikimuingiza Habib Kyombo na Kibu Dennis katika nafasi za Pape Sakho na Augustine Okrah.
Kutokana na matokeo hayo timu hizo bado zimeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu nchini zikiwa na alama 14 kila mmoja katika michezo sita ya ligi kuu nchini.