Kiungo wa klabu ya Yanga sc Khalid Aucho yuko fiti baada ya kupata nafuu katika majeraha yake aliyoyapata wakati wa mchezo wa kombe la shirikisho dhidi ya Real Bamako uliofanyika nchini Mali mwishoni mwa wiki iliyopita hali iliyosababisha ashindwe kuendelea na mchezo huo.
Kiungo huyo baada ya kupata majeraha hayo alitolewa nje na nafasi yake ilichukuliwa na Stephane Aziz Ki huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa na hofu huenda akakaa nje ya uwanja kwa muda mrefu ilhali klabu hiyo inamuhitaji hasa katika michuano hii ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Daktari wa Yanga Moses Etutu amesema kiungo wa kimataifa wa Uganda, Khalid Aucho anaendelea vizuri baada ya kupata jeraha kwenye mchezo huo dhidi Real Bamako ya Mali ambapo Yanga sc ilifanikiwa kupata alama moja.
“Tulidhani amepata jeraha la goti, lakini baada ya kumuangalia tukagungua alipata michubuko mikali chini ya goti baada ya kukanyagwa,Tumempatia matibabu na anaendelea vizuri kabisa hivyo Sio jeraha la kumfanya akose mchezo kwenye mechi zinazofata,”
Kiungo huyo amekua msaada mkubwa katika eneo la kiungo la klabu ya Yanga sc tangu asajiliwe klabuni hapo miaka miwili iliyopita ambapo amefanikiwa kuipa klabu hiyo mataji mawili ya ngao ya hisani pamoja na ligi kuu huku pia msimu huu akisababisha timu hiyo ibaki kileleni mwa msimamo wa ligi kuu.