Klabu ya Tanzania Prisons imelazimisha sare dhidi ya Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu nchini uliofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya baada ya mchezo kumalizika kwa 1-1.
Mchezo huo ulikua wa wazi kwa pande zote mbili kuweza kuibuka na ushindi kutokana na kila timu kujitahidi kuonyesha uwezo wake huku Azam Fc wakitawala mchezo lakini makosa ya kiulinzi yaliwagharimu mapema dakika ya 5 ya mchezo baada ya kuruhusu bao la Samson Mbangula ambaye alipiga shuti kali lililomshinda kipa Mohamed Mustapha.
Licha ya Azam Fc kujitahidi kushambulia kupitia pembeni kwa Gibril Sylla na Kipre Junior mambo yalikua magumu na kuwalazimu kusubiri dakika ya 54 baada ya Jumanne Elifadhil kuunawa mpira na mwamuzi kuamuru pigo la penati iliyofungwa na Feisal Salum ambaye sasa amefikisha mabao tisa katika ligi kuu.
Azam Fc baada ya hapo walijitahidi kushambulia kwa nguvu lakini uimara wa Prisons hasa safu ya ulinzi iliyokua chini ya Nurdin Chona kuzuia hatari zote kwa dakika zote zilizosalia mpaka mpira ulipokwisha.
Kutokana na matokeo hayo Azam Fc imepata sare ya tatu mfululizo katika ligi kuu ikianza na sare dhidi ya Simba sc kisha Tabora United na sasa dhidi ya Tanzania Prisons na imefikisha alama 37 katika nafasi ya pili ya msimamo huku ikiwa imecheza jumla ya michezo 17 na Tanzania Prisons imefikisha alama 21 nafasi ya 7 ya msimamo wa ligi kuu nchini ikiwa imecheza michezo 17.