Mshambuliaji wa klabu ya Yanga Sc Clement Mzize, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa wiki wa michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika na Shirikisho la Soka Afrika (CAF)
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 amekuwa akivutia vilabu vingi vikubwa kutoka nje na ndani ya Afrika kwa muda mrefu na ameendelea kujijengea sifa kwa bora anaozidi kuuonyesha katika miezi ya hivi karibuni.
Magoli yake mawili dhidi ya Tp Mazembe yamefanya idadi ya mabao yake katika Ligi ya Mabingwa msimu huu kufikia matatu katika mechi tatu alizocheza (huku mechi mbili akianza), na yameweka hai matumaini ya Yanga kufuzu hatua ya robo fainali.
Goli lake la kwanza lilikuwa shuti la mbali la kuvutia kutoka mita 30, lililoelekea moja kwa moja kwenye kona ya juu ya wavu ambalo lilisawazishia Yanga kabla ya kufunga goli la pili na kutoa pasi ya mwisho iliyozaa goli moja huku Aziz Ki akiifungia Yanga goli moja na kuweka idadi ya goli 3-1 katika mechi ya nne ya hatua ya makundi iliyopigwa wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam.
Pamoja na kusaidia klabu yake kupata ushindi huo mnono bado ana kazi kubwa ya kufanya kutokana na kuwa na mchezo muhimu wa kuibuka na ushindi ili kuweka mazingira bora ya kufuzu robo fainali ya kundi A la michuano ya klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Al Hilal Omdurman nchini Mauritania.