Connect with us

Makala

Yanga Sc Yabeba Ngao ya Jamii

Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuchukua taji la kwanza la msimu baada ya kubeba taji la Ngao ya jamii katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kuilaza Azam Fc kwa mabao 4-1.

Kocha wa Azam Fc Yousouph Dabo anastahili law lawama baada ya kuamua kuanza na mabeki watatu huku akiweka viungo wanne na washambuliaji watatu mfumo ambao ulimrahisishia kazi kocha wa Yanga sc Miguel Gamondi.

Mabeki Yanick Bangala,Yoro Diaby na Yeison Fuentes walishindwa kuendana na kasi ya Yanga sc ikiongozwa na Prince Dube aliyeshirikiana vyema na Stephan Aziz Ki sambamba na Pacome Zouzoua.

Feisal Salum aliwatanguliza Azam Fc dakika ya 14 ya mchezo akipokea pasi ya Gibril Sillah aliyemzidi maarifa Maxi Nzengeli na kumkuta mfungaji huku Djigui Diarra akiwa hana la kufanya.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 4 tu ambapo Prince Dube alisawazisha dakika ya 18 kwa pasi safi ya Mudathir Yahaya iliyopenyezwa kiufundi zaidi na kuwapita mabeki wa Azam Fc.

Nzengeli tena alipiga pasi nzuri ya kupenyeza kwa Chadrack Boka aliyepiga krosi safi ambayo ilisababisha beki Yoro Diaby kujifunga dakika ya 27 huku dakika tatu baadae Stephan Aziz Ki aliwazidi maarifa walinzi wa Azam Fc na kupiga shuti lililojaa wavuni na kufanya Yanga sc waende mapumziko wakiwa 3-1.

Kocha Dabo aliamua kurudi kwenye mfumo wa mabeki wanne lakini tayari Gamondi alikua kashamaliza biashara na kuamua kucheza kwa kuupooza mchezo ili kulinda ushindi wake.

Kuingia kwa Cletous Chama kulileta matokeo kwa Yanga sc ambapo dakika za nyongeza alitoa pasi safi kwa Mzize aliyefunga bao la nne kwa Yanga sc na kuzua shangwera za kutosha hasa baada ya mwamuzi Ahmed Arajiga kupuliza filimbi ya mwisho.

Yanga sc baada ya kuchukua ngao hiyo ya nane tangu ianzishwe mwaka 2001 sasa itaenda kucheza michuano ya Kombe la klabu bingwa hatua ya awali ambapo itavaana na Vital O ya Burundi mwishoni mwa wiki hii.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala