Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuingia mkataba mnono wa udhamini na kampuni ya Karimjee Mobility kupitia kampuni ya Hero ambayo inatengeneza pikipiki na kusambaza ambapo Kampuni ya Hero inatajwa kuwa kampuni namba 1 duniani kwa biashara hiyo ikiwa imesambaa zaidi ya nchi 40 duniani.
Kampuni itaipa Yanga sc kiasi cha shilingi milioni mia tatu kutokana na mkataba huo wa miezi 18 ambapo wanachama wa klabu hiyo watapata kamisheni endapo watasaidia kuleta wateja kupitia matawi mbalimbali ya klabu hiyo yaliyoenea nchi nzima.
“Leo tumeingia makubaliano na kampuni ya Karimjee Mobility kupitia kampuni ya Hero ambayo inatengeneza pikipiki na kusambaza. Kampuni ya Hero inatajwa kuwa kampuni namba 1 duniani kwa biashara hiyo. Kampuni hii kutoka India inafanya biashara mataifa zaidi ya 40. Young Africans SC itapata kiasi cha Tsh Milioni 300 kutoka kwenye mkataba huu katika kipindi cha miezi 18” Alisema Rais wa Yanga SC Eng. Hersi Said
Naye Meneja masoko wa kampuni hiyo Nadah Dhiyeb alisema kuwa wanajivunia kuingia mkataba na klabu hiyo yenye heshima nchini ambapo wao kama kampuni wanaamini mpango huo utafanikiwa kupitia matawi mbalimbali ya klabu hiyo.
“Tunajivunia kuingia mkataba na Klabu yenye heshima kubwa sana katika historia ya soka la Tanzania. Tunajua muungano huu kupitia matawi ya Young Africans SC tutapanua wigo wa biashara yetu kwa kuweka mtandao mkubwa” Alisema Nadah Dhiyeb – Meneja Masoko Karimjee Mobility.
Yanga sc imefanikiwa kuingiza mamilioni ya pesa kupitia wadhamini mbalimbali wanaominika klabuni hapo ambapo inajumuisha kampuni ya Sportspesa ambao ni wadhamini wakuu huku kukiwa na wadhamini wengine kama Gsm,watercom,nic na wengine.