Winga wa klabu ya Simba sc Leandre Willy Onana ameing’arisha klabu hiyo katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika baada ya kuipatia alama tatu muhimu katika mchezo dhidi ya Wydad Athletics uliofanyima katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
Onana katika mchezo ambao alianza kama winga wa kushoto alifunga mabao mawili muhimu na kuipatia klabu yake ushindi wa 2-0 ambapo alifunga mabao hayo dakika za 36 na 38 kwa ufundi mkubwa akipokea pasi za Kibu Dennis na Mzamiru Yassin.
Simba sc iliyoingia katika mchezo huo bila nyota wake Moses Phiri,Saido Ntibanzokiza na Sadio Kanoute ilianza na mabeki wa kila siku wakiongozwa na Henock Inonga na Che Fondoh Malone huku pembeni wakianza Mohamed Hussein na Shomari Kapombe na Mzamiru Yassin,Fabrice Ngoma na Cletous Chama wakiwa eneo la kiungo huku Kibu Dennis,Onana na Jean Baleke wakiongoza mashambulizi.
Kipa Ayoub Lakred alikua na mchezo mzuri kwa dakika zote tisini ambapo aliiweka Simba sc mchezoni mara kadhaa akifanya uokozi mzuri wa mashuti makali ya Wydad hasa kipindi cha kwanza cha mchezo huo akiokoa hatari za Boully Sambou.
Kipindi cha pili ili kulinda ushindi kocha Benchika aliamua kuwaingiza mabeki Israel Mwenda,Kennedy Juma,David Kameta huku akijaza pia viungo wa ulinzi akimuinga Khamis Abdalah ili kulinda ushindi huo ambapo mpango huo ulifanikiwa.
Simba sc sasa imefikisha alama tano katika nafasi ya pili ya kundi B baada ya kucheza michezo minne huku Asec Mimosa ikifikisha alama 10 kileleni mwa msimamo na Jwaneng Galaxy ikiwa na alama nne huku Wydad wakisaliwa na alama tatu.