Klabu ya Simba sc imefanikiwa kuinasa saini ya kocha Abdelhak Benchikha kwa mkataba wa miaka miwili akichukua nafasi ya kocha Robertinho ambaye aliacha kibarua cha kuinoa Simba Novemba 07, 2023 kwa makubaliano ya pande mbili.
Kocha huyo anakuja katika kipindi ambacho klabu hiyo inasumbuliwa na mzimu wa kufungwa 5-1 na Yanga sc huku uzoefu wake wa kufundisha vilabu 24 barani Afrika ukitajwa kama moja ya sababu ya kuwa kocha imara na asiyefungika kirahisi.
Benchika atakumbukwa na Yanga sc baada ya kupoteza Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya USM Alger akiwafunga 2-1 nyumbani licha ya klabu hiyo kugeuza kibao na kushinda 1-0 ugenini.
Tayari kocha huyo licha ya kuwa alitambulishwa Ijumaa usiku, akiwa kwao Algeria na Jumamosi alianza safari ya kuja Bongo huku leo Jumatatu anatarajiwa kuwa ataanza rasmi kazi ndani ya kikosi hicho ambapo amewataka mastaa wote kuripoti kambini haraka.
“Naijua Simba ni timu nzuri na imekuwa na ushindani mkubwa katika bara hili la Afrika, nina furaha kujiunga nao. Kwa sasa siwezi kusema chochote kuhusu mipango yangu binafsi, naenda kutimiza mipango ya timu kutokana na makubaliano yetu,” amesema Benchikha na kuongeza;
“Kitu cha kwanza nitakachofanya ni kukutana na wachezaji wote kambini, nataka nionane na kila mmoja na kutambua uwezo wake na baada ya hapo nitaanza kutengeneza timu nikiendeleza nilipoikuta.”
Benchikha ataanza kuiongoza Simba kwenye mechi ya michuano ya CAF, itakayopigwa Desemba 2 ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ukiwa ni mchezo wa pili kwenye kundi la timu hizo lenye Wydad Casablanca ya Morocco.