Connect with us

Makala

Simba sc Kumaliza Kazi Dar

Baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Power Dynamos ya nchini Zambia sasa klabu ya Simba sc inajipanga kuja kuumaliza mchezo huo jijini Dar es salaam wakati wa marudiano ili kukata tiketi ya kuingia hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika.

Simba sc ikiwa ugenini ilijikuta ikilazimishwa sare na wenyeji ambao walikua na mchezo mzuri pamoja na kasi zaidi hasa wanapoenda kushambulia hasa kupitia pembeni alipokua anacheza winga Joshua Mutale ambaye alisababisha goli la kwanza dakika ya 28 baada ya kuingia kwenye eneo la 18 kwa nguvu na kupiga krosi iliyomfanya Henock Inonga ajifunge.

Cletous Chama alionyesha ukubwa wake baada ya kufunga goli la kusawazisha akiunganisha mpira uliotemwa na kipa wa Dynamos kutokana na shuti kali la Mzamiru Yassin dakika ya 59.

Makosa ya kipa Ayoub Lakred yaliwapa Dynamos goli la pili baada ya kushindwa kucheza shuti la Cleophas Mulombwa na kuwapa wakati mgumu mashabiki wa klabu hiyo waliojazana uwanjani hapo huku wengine wakiwa wametoka jijini Dar es salaam.

Chama tena aligeuka mwokozi baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa Simba sc akipiga shuti kali lililomshinda kipa Lawrence Mulembwa na kurudisha matumaini ya Simba sc kufuzu hatua ya makundi kwa mara nyingine tena wakifanya hivyo hata mwaka jana.

Hata hivyo kocha wa klabu hiyo Roberto Oliveira maarufu kama Robertinho amewapongeza wachezaji kwa kazi kubwa waliyofanya katika mchezo wa jana licha ya kupata sare.

“Tumecheza vizuri hasa kipindi cha pili, tumetengeneza nafasi nyingi. Tumepoteza nafasi zaidi ya tano za kufunga lakini huu ndio mpira wa miguu tunarudi nyumbani kujipanga,” amesema Robertinho.

Kwa upande wake mlinzi wa kati wa klabu hiyo Che Fondoh Malone amesema bado wanafasi ya kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam hivyo wanarudi kujipanga.

“Hatujakata tamaa ya kusonga hatua ya makundi, tuna dakika 90 nyingine nyumbani ambazo tunaamini tutazitumia vizuri na kuingia hatua ya makundi,” amesema Che Malone ambaye ni raia wa Cameroon.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala